WILLIAM MARRION BRANHAM (1909-1965)

William Marrion Branham alikuwa mhubiri wa Biblia mwenye ushawishi mkubwa wa wakati wetu, anayechukuliwa na kuaminiwa na wengi kuwa mwanzilishi wa uponyaji na uamsho ulioanza mwaka 1947.

Kuanzia mwaka 1947 hadi wakati wa kifo chake mwaka 1965, huduma yenye nguvu ya William Branham ilikuwa maarufu na inachukuliwa kuwa isiyo na kifani katika historia ya mikutano ya Injili. Matokeo ya huduma ya kimiujiza ya mtu huyu ilitambuliwa si tu Amerika Kaskazini, bali pia ulimwenguni kote.

Maelfu ya visa vilivyothibitishwa vya kila namna ya uponyaji vilidhihirishwa katika Marekani, Kanada, Afrika, na kote ulimwenguni kupitia maombi ya William Branham.

Vipofu walipata kuona, wagonjwa wa saratani waliponywa, vilema, na wale wasioweza wakaponywa kabisa.  Hakuna ugonjwa uliosimama njiani kama Mungu alivyothibitisha kwa mamilioni, kwamba Yeye angali ni Mungu leo, yeye yule jana, leo na hata milele (Waebrania 13:8) katika huduma ya mjumbe Wake wa wakati wa mwisho kwa wakati wetu.

Lakini muhimu zaidi, William Branham alituleta Ujumbe wa wakati wa Mwisho uliorejesha mambo yote yaliyokuwa hayajakamilika katika Biblia ambayo, hata kama vyuo vyote vya Biblia duniani vingekusanywa pamoja, kamwe visingeweza kutufunulia. Mafundisho haya ni pamoja na Fumbo la uungu wa Mungu, Ukweli kuhusu Ubatizo kwa Maji, Dhambi ya Asili, Kuchaguliwa kimbele, Ufunuo wa Mihuri Saba, Kuzaliwa Upya, Alama ya Mnyama, Fumbo la Babeli. Hizo kweli zimerejeshwa kwa kanisa leo ili kuandaa Bibi wa Yesu Kristo katika kila taifa kujiandaa kwa Unyakuo, ambao ni kurudi kwa pili kwa Bwana.

William Branham alisema:

“Ama wajiunge na kanisa langu, ama waanzishe shirika fulani na madhehebu fulani. Sijafanya hivyo kamwe wala sitafanya hivyo sasa. Sivutiwi na mambo hayo, bali ninavutiwa na mambo ya Mungu pamoja na watu, na kama naweza kutimiza jambo moja tu nitaridhika. Jambo hilo moja ni kuona uhusiano wa kweli wa kiroho baina ya Mungu na watu umeimarishwa, ambapo watu wanakuwa viumbe vipya katika Kristo, wamejazwa na Roho Wake na wanaishi kulingana na Neno Lake. Ningewaalika, ningewasihi na kuwaonya watu wote waisikie sauti Yake wakati huu, na kuyatoa maisha yenu kabisa Kwake, yaani kama vile ninavyoamini moyoni mwangu kwamba nimempa Yeye yote niliyo nayo. Mungu na awabariki, kuja Kwake na kuifurahishe mioyo yenu.”

 MASHAHIDI WA HUDUMA YA BRANHAM.


Zifuatazo ni shuhuda zilizothibitishwa kutoka kwa wahubiri na wainjilisti maarufu duniani kote kuhusu huduma ya William Marrion Branham:

JAMES MORRIS – “Ilikuwa ni Branham, zaidi ya mwinjilisti mwingine yeyote, aliyeanzisha uamsho na uponyaji mara baada ya Vita vya pili vya dunia, kufuatia kukutana kwake na malaika mnamo Mei 7, 1946. Neno lilienea kila upande kiasi kwamba aina zote za magonjwa na mateso  yaliponywa papo hapo na yule mhubiri mdogo wa Indiana.  Hata visa vya kufufua wafu vilichapishwa.”  (-The Preachers)

GORDON LINDSAY – “Hatukuwahi kujua kuhusu mhubiri yeyote anayeweza kuwaita viziwi, bubu na vipofu awaombee, na kisha kuona watu hao wakipokea uponyaji mara moja… huduma ambayo ilikuwa zaidi ya yoyote tuliowahi kuishuhudia hapo awali.”  (-The House that the Lord Built)

TOMMY OSBORN – “Mungu amechagua njia mbalimbali na za ajabu ili kujidhihirisha Mwenyewe kwa watumishi Wake hasa wale walioitwa kwa madhumuni maalum, kwa kipindi fulani kama vile wito wa Ndugu Branham.  Kwa ufupi, mtu tunayemjua kama William Branham alitumwa kuonyesha Mungu tena katika mwili.  (-William Branham Memorial Service)

JACK MOORE – ‘Mwenye kipawa zaidi kati ya wainjilisti wote.’ (-All Things are Possible na David Harell, Jr.)

ORAL ROBERTS – “Mtu mnyenyekevu mwenye imani kwa Mungu.” (-Healing Waters, Julai 1948)

F.F. BOSWORTH – “Wakati kipawa kinapotenda kazi, Ndugu Branham ni mtu mwenye ufahamu zaidi wa uwepo na kazi ya Roho Mtakatifu na ukweli wa kiroho kuliko mtu yeyote niliyemfahamu.” (-A Prophet Visits South Africa)

GEORGE EKEROTH – “Mungu alimwita mtu mnyenyekevu huyu na kumtia mafuta kwa huduma yake kwa kiwango ambacho ndani ya miaka michache fupi jina lake lilijulikana katika vituo vya mbali sana vya msituni. Popote unapokwenda katika ulimwengu huu, utagundua kwamba jina la mjumbe huyu limekwisha kutangulia mbele yako.” (-Utangulizi wa Kitabu cha Morris Cerullo, Wind Over the 20th Century)

GEORGE EKEROTH – “Mungu alimwita mtu huyu mnyenyekevu na kuipaka mafuta huduma yake kwa kiwango ambacho ndani ya miaka michache jina lake lilijulikana katika maeneo ya vijijini zaidi. Popote unapoenda katika ulimwengu huu utapata kwamba jina la Mtume huyu limekutangulia. “(-Introduction of Morris Cerullo’s Book, Wind Over the 20th Century)

DAVID EDWIN HARRELL JR. – “Wengi wa washiriki wa uponyaji ulioibuka mwaka 1947 walimtazama Branham kama mwanzilishi wake. William Branham akawa nabii kwa kizazi kizima. Usiku baada ya usiku, mbele ya maelfu ya waamini walioogopa, aligundua magonjwa ya wagonjwa na kuwatangazia kuponywa. Nguvu ya huduma ya Branham inabaki hadithi isiyolinganishwa katika historia ya Harakati ya Charismatic.” (-All Things Are Possible)

DAVID EDWIN HARRELL JR. – “Wengi wa washiriki wa uamsho wa uponyaji ambao ulianza mwaka 1947 walimtazama Branham kama mwanzilishi wake. William Branham akawa nabii kwa kizazi. Usiku baada ya usiku, mbele ya maelfu ya waumini waliojawa na mshangao, alitambua magonjwa ya wagonjwa na kuwatangazia uponyaji. Nguvu ya huduma ya Branham bado ni hadithi isiyoweza kulinganishwa katika historia ya harakati ndani ya baadhi ya makanisa ya Kikristo ambayo yanasisitiza karama zinazoaminika kutolewa na Roho Mtakatifu, kama vile kunena kwa lugha na uponyaji wa wagonjwa.. “ (- All things  are possible)

THOMAS R. NICKEL – “Katika siku za Biblia, kulikuwa na Watu wa Mungu ambao walikuwa manabii na waonaji. Lakini katika rekodi zote za kitakatifu, hakuna hata mmoja wao aliyekuwa na huduma kubwa kuliko ile ya William Branham, Nabii na Muonaji wa Mungu, ambaye picha yake inaonekana kwenye ukurasa wa mbele wa jarida hili la Full Gospel Men’s Voice. Branham ametumiwa na Mungu, kwa jina la Yesu, kuwafufua wafu.” (-Jarida la Full Gospel Men’s Voice, Februari 1961)

JOSEPH MATTSON-BOZE – “Wakati mwingine nilikuwa naogopa kutokana na mguso mkuu wa utakatifu uliopenya kwenye mkutano, lakini kamwe sikushindwa kuona kazi ya Mungu ikifanya kazi kupitia mtumishi wake na kuhisi joto la upendo lililopita kupitia huduma yake.” (-The Herald of Faith, Februari 1966)

MAISHA YA AWALI NA UONGOFU

William Branham alizaliwa Aprili 6, 1909 katika kibanda cha mbao huko kwenye milima ya Kentucky, akiwa mtoto wa kwanza kati ya watoto tisa wa Charles na Ella Branham. Akiwa amelelewa karibu na Jeffersonville, Indiana, alijua maisha ya umaskini mkubwa na na hali ugumu, baba yake akiwa mlevi na asiye na elimu. Akiwa amezungukwa na hali hizi, mvulana huyu mdogo alionekana kuwa “mwenye wasiwasi”, kwa sababu tangu utotoni mwake alikuwa akizungumza juu ya “maono” na “sauti” iliyomzungumzia kutoka kwenye upepo, ikisema, “Kamwe usinywe, wala usivute, wala usiutie unajisi mwili wako kwa njia yoyote. Kutakuwa kuna kazi ya kufanya utakapokuwa mkubwa.”


William Branham alimjua Bwana na kujazwa na Roho Mtakatifu mwaka 1931. Tangu wakati huo, Biblia ilikuwa ndio hasa lengo katika maisha yake na Yesu Kristo alikuwa kitovu cha kuwepo kwake! Aliwekwa wakfu kwa ajili ya huduma akiwa na umri wa miaka 23, katika kanisa la Kibatisti mnamo Desemba ya 1932.

KUJILIWA NA MALAIKA


Tarehe 11 Juni 1933, William Branham alikuwa akibatiza katika Mto Ohio karibu na Jeffersonville, Indiana, mwanga mkali wa moto ulitokea ghafla juu ya kichwa chake na sauti ikasema, "Kama Yohana Mbatizaji alivyotumwa kuutangulia ujio wa kwanza wa Yesu Kristo, vivyo hivyo wewe umetumwa kuutangulia ujio wake wa pili!" Gazeti la “The evening news” la Jeffersonville liliripoti tukio hilo na kuandika kichwa kidogo cha habari, "Nyota Isiyoeleweka Yazuka Juu ya Mhubiri Wakati wa Kubbatiza."

Mnamo Mei ya 1946, alijiweka kando kumtafuta Mungu ili kutaka kujua hasa sababu za ya maisha yake ya ajabu. Alipokuwa akiomba peke yake usiku mmoja, malaika wa nuru alionekana, akisema, “Usiogope. Nimetumwa kutoka kwenye uwepo wa Mungu Mwenye Nguvu kukujulisha kwamba kuzaliwa kwako kipekee na maisha yasiyoeleweka imekuwa ni ishara kwamba wewe unapaswa kuleta cha uponyaji wa kiungu kwa watu duniani. Ikiwa utakuwa mwaminifu unapomwomba Mungu na kuwafanya watu wakuamini, hakuna kitu kitakachosimama mbele ya maombi yako, hata kansa. Utazunguka sehemu nyingi duniani na kuwaombea wafalme na watawala na wenye nguvu. Utahubiri mbele ya umati mkubwa kote duniani na maelfu watakujia kwa ushauri.”

Kwa nusu saa, malaika huyu alimwelezea Ndugu Branham kuhusu mambo ya wakati uliokwishapita na kumwambia kuhusu mustakabali wake. Alieleza kwa nini wahubiri hawakuweza kutambua karama ya Mungu maishani mwa William, lakini shetani alikuwa na uwezo wa kutambua. Hali ilikuwa kama ile ya siku za Yesu: viongozi wa kidini walisema Yesu ana pepo, lakini mapepo huko Gadara walimtambua (Marko 3:22; Yohana 7:20).

ISHARA MBILI ZILIZODHIHIRISHWA

Malaika pia alimwambia Ndugu Branham kwamba, kama vile Musa alivyopewa ishara mbili kuthibitisha alitumwa na Mungu (Kutoka 4:1-8), vivyo hivyo angepewa ishara mbili. Kwanza, angekuwa na uwezo wa kutambua magonjwa kwa njia ya mitetemo yake, ambayo ingesababisha mkono wake kuvimba. Ikiwa uvimbe ungepungua baada ya kumuombea mtu, angeweza kusema, "Hivi asema Bwana, umeponywa." Malaika alisema wakati ungefika ambapo Ndugu Branham angeweza kutambua siri za mioyo ya watu (Waebrania 4:12; Yohana 2:24-25).

Mamilioni ya watu wanashuhudia kwamba maneno ya malaika yalitimizwa kikamilifu (kama ilivyo katika Matendo 27:21-25). Ishara iliyokuwa mikononi mwake ilidhihirika, na ilipotazamwa ingeinua imani ya watu ya kuponywa, huduma yake ilikua kitaifa, kisha kimataifa. Kisha ikafika mahali ambapo Roho wa Kristo angefunua kwake mawazo halisi ya mioyo ya watu, kufichua mahitaji yao, kufunua dhambi zisizotubiwa ambazo hazikuoshwa na Damu ya Yesu Kristo; kufunua mambo kuhusu maisha yao ambayo Ndugu Branham mwenyewe hangeweza kujua. Si kusoma akili wala saikolojia, bali badala yake angeona maono juu ya hayo – mambo yaliyotendeka mbele ya macho yake wazi (Yoeli 2:28). Na alipozungumza chini ya upako, katikati ya mamia mara maelfu ya watu ulimwenguni kote, maneno aliyoyasema kwa wageni hayakushidwa kamwe kuwa kweli kamilifu. Na unabii – wa uponyaji, wa matukio ya baadaye, madogo hadi makubwa, mara elfu na mara elfu na mara elfu – hata mara moja hakukuwa na kosa hata kidogo! Ilikuwa ni halisi, “HIVI ASEMA BWANA!”

Katika miaka kumi iliyofuata, Ndugu Branham alizunguka dunia mara saba, akifanya mikutano mikubwa zaidi katika historia. Watu takriban 100,000 walimsikia huko Durban, Afrika Kusini. Malori saba yalichukua magongo, viti vya magurudumu, fimbo, n.k., baada ya huduma za uponyaji.

Watu wengi wenye ushawishi kwenye umma, ikiwa ni pamoja na Mbunge Upshaw wa Marekani na Mfalme George VI wa Uingereza, waliponywa kutokana na sala zake.

HUDUMA ULIMWENGUNI KOTE

Habari za miujiza na uponyaji zilipoenea, wachungaji kutoka sehemu zote walianza kumwita Ndugu William Branham awahudumie kwenye makusanyiko yao na kuwaombea wagonjwa. Alikuwa amepewa Ishara ya kimiujiza kwa lengo la kuwatia moyo watu wamwamini.

Kwanza, ishara ya kimwili kwenye mkono wake ingeonyesha ugonjwa au uponyaji. Baadaye katika huduma yake, mawazo na mahitaji ya siri za watu binafsi yalifunuliwa, na hivyo kupelekea imani ya uponyaji. Ilikuwa wazi kwa msomaji yeyote wa Biblia kwamba William Branham alikuwa ametiwa mafuta kuwa nabii kutekeleza unabii wa Maandiko mengi kuhusu wakati wetu. Makanisa hayakuweza kumudu umati wa watu, na mikutano ilihamia kwenye majengo makubwa au viwanja vya michezo kwa kampeni za pamoja katika miji mikubwa ya Amerika Kaskazini.

Wakati akihubiri Injili ya Yesu Kristo huko Portland, Oregon, mwanaume mwenye pepo alikwea jukwaani, akimuita Ndugu Branham mwongo, bandia, mwendawazimu, akitishia kuvunja kila mfupa mwilini mwake. Mtu huyo alipokaribia kutekeleza vitisho vyake, Ndugu Branham alisema kwa upole, “Shetani, kwa sababu umemkataa mtumishi wa Mungu – kwa Jina la Yesu Kristo, utaanguka miguuni mwangu.” Mwanaume mwenye nguvu alijaribu kukaribia zaidi, lakini hakuweza. Alianguka chini na ilibidi abebwe na waangalizi wa ibada kwa sababu aliangukia uso mbele ya mtumishi wa Mungu aliyethibitishwa na Mungu.

Huko Bombay, India, ambapo watu takribani 400,000 walikuja kusikia Injili, kulikuwa na kipofu ombaomba aliyekuja mbele ya Ndugu Branham ili aweze kuombewa. Katika maono, Ndugu Branham aliona kuwa huyu omba omba alikuwa nani, alikuwa anakaa wapi, na kwamba alikuwa kipofu kwa sababu ya kutazama jua, ambalo aliliabudu kama Mungu wake. Kisha Ndugu Branham aliwakaribisha makuhani mbalimbali wa Kihindu kwa zamu akisema, “Ikiwa mungu wenu ni Mungu, basi njoo hapa jukwaani na mmwambie afungue macho ya mtu huyu, na akiweza tutaona na kumsujudia huyo mungu wenu.” Hakuna thubutu kusogea. “Lakini ikiwa Mungu wangu, Bwana Yesu Kristo, ni Mungu na atafungua macho ya mtu huyu, je, mtaiacha miungu yenu isiyokuwa na nguvu na kumkubali Yesu kama Mwokozi wenu?” Walikubaliana na hilo. Sababu ya kujiamini kwa Nabii huyu ilikuwa kwa sababu alikuwa ameshaona uponyaji wa huyu mtu kwenye ono, na maono haya kamwe hayakumwacha. Wakati macho ya mwombaji yalipofunguka na kuona watu wote katika mkutano huo, ghasia ziliibuka huku watu maskini wakijitahidi kumgusa Ndugu Branham ili kuponywa.

Ilikuwa huko Mexico ambapo imani ya mwanamke ilisababisha Mungu kufanya muujiza mkubwa. Daktari aliandika taarifa ya kiapo kwamba mtoto wake alikufa saa 9:00 asubuhi kutokana na nimonia, lakini kwa sababu alikuwa amemwona Mungu akimrudishia mwanaume kipofu uwezo wa kuona katika mikutano ya Ndugu Branham usiku uliotangulia, aliendelea kubeba mtoto wake aliye kufa mchana kutwa, akiamini kwamba angefanikiwa kumfikisha kwa Ndugu Branham, Mungu angefufua. Usiku huo, ambapo Ndugu Branham alikuwa na mkutano, aliona maono ya mtoto wa Kimeksiko akibebwa na mama yake, akiwa hai. Hapo aliomba kwa jina la Yesu na kuweka mikono juu ya mtoto. Mara moja mtoto huyo alianza kulia kwa kuwa alikuwa amerejeahewa tena uhai. Habari hiyo iliandikwa kwenye makala na daktari aliyetoa cheti cha kifo hakuweza kuamini kilichotokea.


NGUZO YA MOTO


Picha ambayo upande wake wa kushoto kuna NGUZO YA MOTO juu ya kichwa cha Ndugu Branham ilichukuliwa huko Houston, Texas, mwezi wa Januari mwaka 1950. Nuru hii ilikuwa ikiambatana na Ndugu Branham tangu kuzaliwa kwake mwaka 1909. Na wakati wa huduma ya ubatizo mwaka 1933 katika Mto Ohio huko Jeffersonville, Indiana, KIUMBE HIKI CHA KIMBINGUNI kilitokea mbele ya mamia ya watu kikimwambia, “Kama Yohana mbatizaji alivyotangulia kuja kwa Kristo mara ya kwanza, wewe utatangulia kuja kwake mara ya pili.” Picha hii inaoneshwa leo katika Maktaba ya Congress huko Washington, D.C. na ilifanyiwa uchunguzi na kuthibitishwa kuwa halisi na Bwana George Lacy, mtathmini wa Nyaraka zenye viulizo/mashaka nchini Marekani, kuwa hati pekee ya kweli ya nguvu za kiungu katika kizazi hiki.

WINGU LA AJABU

Mnamo Februari 28, 1963, huko Arizona, Marekani, kundi nyota la malaika saba lilimtokea Mchungaji William Marrion Branham kwa mfumo wa wingu lenye umbo la pete.

Hawa malaika saba walitoka mbele za Mungu wakimfunulia siri zilizofichwa za Biblia zilizokuwa zimetiwa mhuri katika Kitabu cha Danieli na Kitabu cha Ufunuo, ingawa zilikuwa zimewekwa wakfu kufunuliwa wakati wa mwisho. Hii ilikuwa kwa lengo la kuwajulisha watu wa Mungu kuhusu mapenzi kamili ya Baba katika maandalizi ya utawala wa milenia wa Yesu Kristo juu ya dunia hii.

Ilivyokuwa walipoondoka machoni pa Ndugu Branham ndipo walipounda hili wingu la ajabu ambalo lilichapishwa kwenye Jarida la Life toleo lao la Mei 17, 1963, na Jarida la Sayansi katika toleo lao la Aprili 19, 1963.


Picha asilia zenye mwangaza zinaonyesha uso kamili wa Bwana Yesu Kristo huku picha ikionekana kutoka pembeni kulia “kama Mwana wa Adamu, kichwa chake na nywele zake zilikuwa nyeupe kama sufu, nyeupe kama theluji” (Ufu. 1:13).

Vitabu saba vya ufunuo vilivyotiwa muhuri vilifunuliwa

Mnamo Desemba 22, 1962, Ndugu Branham aliona ono alipokuwa amesimama karibu na Tucson, Arizona, alikuwa akitoa mchanga kwenye suruali yake, wakati mlipuko mkubwa ulitokea. Alieleza ono hili kwa waumini wake huko Jeffersonville, Indiana mnamo tarehe 31 Desemba (mahubiri yalirekodiwa kwenye kanda). Baadaye akahamia Tucson, Arizona.

Zaidi ya mwezi mmoja baadaye, tarehe 28 Februari, 1963, alipokuwa akienda kuwindwa, aliona mchanga kwenye suruali yake. Alipoinua mkono kuitoa, mlipuko mkubwa ulitikisa upande wa mlima. Akiangalia juu, aliona malaika saba wakija kwake kwa mfumo wa piramidi, na kwa muda alionekana kusimama katikati yao. Hawa malaika saba wanawakilisha Wajumbe Saba wa Nyakati Saba za Kanisa kama ilivyoandikwa katika Ufunuo sura ya 2 na 3.

Kisha sauti ikapaza, “Rudi upande wa mashariki,” na Ndugu Branham alijua ilikuwa wakati wa kufunuliwa kwa siri za Mihuri Saba katika Kitabu cha Ufunuo (Danieli 12:4,8-9; Ufu. 5,6 na 8) ambazo malaika walimkabidhi. Malaika walirudi angani na kuunda wingu lenye urefu wa maili 50 na upana wa maili 30, ambalo lilikuwa linaweza kuonekana kwa mamia ya maili mbali.

Picha nyingi za Wingu hili la kipekee zilichukuliwa, baadhi zilichapishwa katika Jarida la Life (toleo la Mei 17, 1963); nyingine katika Jarida la Sayansi (toleo la Aprili 19, 1963), pamoja na ripoti ya kisayansi jinsi ilivyokuwa haiwezekani kisayansi kwa wingu kama hilo kuwepo. Wingu la juu zaidi hujitokeza takribani maili 10, lakini wingu hili la kushangaza lilikuwa maili 26 juu, ambapo unyevunyevu wa maji hauwepo.

Ndugu Branham alirudi Jeffersonville, Indiana ambapo kwa siku saba, akimngojea Mungu, sauti ya Mungu iliongea kupitia Nguzo ya Moto, ikifunua Ukweli kamili wa Siri zilizofungwa katika Ufunuo 5 hadi 8; ufunuo ambao ulikuwa kinyume na ule ambayo kila mtu (ikiwa ni pamoja na Ndugu Branham) alikuwa amefikiria awali, lakini ulikuwa kamili kulingana na Neno lote la Mungu.

Kama Ndugu Branham alihubiri siku saba mfululizo kuhusu hizi Mihuri (Machi 17-24, 1963), mahubiri yake yalirekodiwa kwenye sauti: Hivyo Maandiko yanatimia katika siku zetu yakisema, “Lakini isipokuwa katika siku za sauti ya malaika wa saba atakapokuwa tayari kupiga baragumu; hapo ndipo siri ya Mungu itakapotimizwa, kama alivyowahubiri watumishi wake hao manabii.” (Ufu. 10:7).

MAONO SABA YA WILLIAM BRANHAM

Katika mwaka wa 1933, Mungu alimpa Ndugu Branham maono mwendelezo ya mambo saba makuu ambayo lazima yatokee kabla ya Bwana Yesu Kristo kuja tena.

Ono la kwanza (1) ilikuwa kwamba aliona dikteta akiinuka nchini Italia ambaye angeivamia Ethiopia.  Alimwona Mussolini na mwisho wake wa aibu ambapo watu walimgeukia, kabla haijatokea katika tukio halisi.

Ono la pili (2) alionyeshwa na Mungu ambapo alimwona kijana Mwaustria aliyeitwa Adolf Hitler ambaye angepata mamlaka/nguvu nchini Ujerumani na angeuibgiza ulimwengu kwenye vita, na kwamba Ujerumani ingeshindwa na Hitler angefikia mwisho wa kutatanisha.

Katika ono la tatu (3), aliona ITIKADI tatu kuu ulimwenguni: Ufashisti, Unazi na Ukomunisti: lakini zile mbili za kwanza zingemezwa na ile ya tatu – Ukomunisti.

Kisha katika ono la nne (4), aliona maendeleo makubwa sana ya sayansi ambayo yangefuatia baada ya vita vya Pili vya Dunia.  Aliona gari likionekana kama yai ambalo linaendeshwa si na wanadamu bali kwa udhibiti wa mbali (Rimoti).

On la tano (5)   alioneshwa upotovu wa kutisha wa kimaadili duniani, hasa kwa wanawake.  Aliwaona wanawake wakikata nywele zao, wakivuta sigara, wakinywa pombe, wamevaa suruali na mavazi yasiyofaa.  (Kumbuka mambo haya matano alionyeshwa mwaka 1933, miaka kadhaa kabla hayajatokea).

Katika ono la sita (6), aliona mwanamke mrembo, lakini mkatili akiinuka Marekani, akitawala nchi kwa mamlaka.

Na katika ono la mwisho (7), aliona nchi ya Marekani katika magofu yanayofuka moshi.  Kwa kadiri macho yalivyoweza kuona hapakuwa na uhai, ila mashimo tu na marundo yanayofuka moshi.  Pia aliona Los Angeles, California ikizama chini ya bahari kutokana na tetemeko kubwa la ardhi.  Kisha maono haya yakapotea.

UNABII ULIOTIMIA KATIKA SIKU ZETU

“Hakika Bwana MUNGU hatafanya neno lo lote, bila kuwafunulia watumishi wake manabii siri yake.” Amosi 3:7

Mpango wa Mungu wa kushughulika na watu wake daima umehusisha kutuma manabii. Nabii Amosi anatuambia kwamba Mungu hafanyi “jambo lolote” bila kuwa na mtangulizi nabii, na hata utafiti wa haraka wa historia ya Maandiko utathibitisha hili kuwa sahihi. Ni mara chache ambapo alitokea nabii kuhubiri neno la Mungu ambaye hakukutana na kutiliwa mashaka, kukataliwa na kutukanwa!

FIKIRIA Maandiko haya juu ya roho ya Eliya:

MALAKI 4:4-6 “Angalieni, nitawapelekea Eliya nabii, kabla haijaja siku ile ya BWANA, iliyo kuu na kuogofya. Naye ataigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto wao, na mioyo ya watoto iwaelekee baba zao, ili nisije nikaipiga dunia kwa laana.”

Malaki 4:5 na 6 ina sehemu mbili, imetimizwa kwa sehemu katika huduma ya Yohana, Mbatizaji.  Alitangulia ujio wa kwanza wa Yesu Kristo, unaoitwa siku “kuu” ya Bwana, akigeuza mioyo ya baba wa “torati” kuelekea watoto wa enzi ya “neema” ya Agano Jipya.

Kama ilivyoelezwa katika Maoni ya Biblia nzima ya Jamieson, Fausset & Brown, “…Yohana mbatizaji alikuwa Eliya katika roho (Luka 1:16,17) lakini si Eliya halisi (Yohana 1:21). Hii ina maana kwamba Yohana, akijua kwamba alitajwa na Malaki 4:5, alijua kwa ufunuo kwamba hakuweza kutekeleza kikamilifu yote yaliyomo katika unabii huo: kwamba kuna kutimiliza zaidi. Kuna nabii atakayetimiza sehemu ya pili ya maandiko haya, akiandaa njia kwa kuja kwa pili kwa Kristo na “kugeuza mioyo ya watoto kuwaelekea baba zao…” Kwa maana halisi, hii inamaanisha kutakuwa na huduma itakayogeza mioyo ya kizazi kilichopotea kurudi kwenye Neno la Mungu na imani ya baba wa “kanisa la mwanzo” kabla ya “siku ya kutisha ya Bwana”, kuja kwa pili kwa Kristo kwa hukumu.

Tena, Mathayo 17:10-12 ina sehemu mbili.  Kwanza, “Mbona basi waandishi hunena ya kwamba imempasa Eliya kuja kwanza?”  “… Lakini nawaambia, ya kwamba Eliya amekwisha kuja wala hawakumtambua…” akizungumzia Yohana Mbatizaji.  Pili, “Na Yesu akajibu, akawaambia, Eliya atakuja kwanza, na kutayarisha mambo yote.”  Akizungumza juu ya mtangulizi wa wakati ujao wa kutangulia kuja kwa pili kwa Kristo.

Huduma ya William Branham ni utimilifu wa ujio wa roho wa Eliya ambao ungetangulia ujio wa pili wa Kristo ambao ni “kurejesha” mioyo ya watoto kwenye mafundisho ya Mababa Mitume.

Huduma ya William Branham ilihusisha hatua tatu tofauti ambazo alizitaja kama “mivuto”.  Mvuto wa Kwanza: Uponyaji.  Mvuto wa Pili: Kutabiri/unabii.  Mvuto wa Tatu: Kufungua au kufunua Neno la Mungu.

Huduma ya Yesu Kristo ilifuata mtindo uleule.  Mvuto wa Kwanza: makundi ya watu yalimiminika ili kusikia maneno yake ya neema na kupokea mguso Wake wa uponyaji wa kimiujiza.  Mvuto wa Pili: Alitambua siri za mioyo.  (Yohana 4:17-18) Mvuto wa Tatu: “Ujumbe” wake, Neno la Mungu lililokuja kwa nguvu kinyume na utaratibu wa kidini wa siku hiyo, na kusababisha umati kumwacha.  “Tangu wakati huo wengi wa wanafunzi wake walirudi nyuma, wasiandamane naye tena.”  Yohana.  6:66

WAJUMBE WA MUNGU WA WAKATI WA MWISHO


NABII HAKOSI HESHIMA ISIPOKUWA KATIKA NCHI YAKE MWENYEWE.

Kwa nini basi William Branham hafahamiki sana leo? Hakuna Nabii wa kweli aliyewahi kukubalika na wengi katika wakati wake. Lakini nabii wa kweli anapinga uovu wa wakati wake, na watu hawapendi kubadilika kutoka njia zao za kimwili. Ni wachache tu watakaofahamu na kuamini, kama ilivyokuwa siku za Yohana Mbatizaji.

Angalia hili: maadamu Yesu Kristo (ambaye alikuwa ni Nabii-Mungu) alipokuwa akiwaponya wagonjwa, umati wa watu ulimsonga.  Lakini alipoanza kutoa mafundisho yenye nguvu, akiwakemea Masadukayo na Mafarisayo (madhehebu ya siku zake), Biblia inasema hivi: “Tangu wakati huo wengi wa wanafunzi wake walirudi nyuma, wasiandamane naye tena,” (Yohana 6:48-68).

Vivyo hivyo, mradi Mungu alimtumia Ndugu Branham kuponya wagonjwa na wanaoteseka, mamilioni walifuata huduma yake.  Lakini Mungu kupitia nabii wake alipoanza kurejesha NENO, watu wengi walipenda miujiza lakini walichukia Neno.  Hata hivyo, Neno lilipaswa kurejeshwa kabla Yesu Kristo hajamchukua Bibi-arusi Wake, kwa maana hana budi kuwa Bibi-arusi wa Neno safi, na maana ya kweli la Neno la Mungu imepotoshwa sana kote katika karne zote mpaka leo;  kama Yesu alivyosema, “Nao waniabudu bure, wakifundisha mafundisho yaliyo maagizo ya wanadamu … wakilitangua Neno la Mungu kwa mapokeo yenu” (Marko 7:6,7,13).

Msidhani ya kuwa mambo hayo humwinua mtu, KRISTO PEKE YAKE AMEINULIWA!  Ndugu Branham mwenyewe hangeweza kufanya lolote (Yohana 3:27).  Ilikuwa ni Yesu Kristo akifanya (kupitia nabii mnyenyekevu) kazi zile zile alizofanya alipotembea katika mwili wa mwanadamu hapa duniani (Ebr. 13:8).  Kwa hiyo usimtazame mtu huyo, bali tazameni Ujumbe aliouleta, kwa maana Ujumbe huo utakuelekeza kwa Yesu Kristo aliye safi, ambaye hafungamani na kanuni na mapokeo yote ya kimadhehebu.

Je, mtume Paulo hakusema, “Iweni wafuasi wangu, kama mimi nilivyo mfuasi wa Kristo,” (1Kor. 11:1; 4:16).  Unapomtii Paulo, humfuati mtu, bali Roho Mtakatifu anayesema kupitia kwake.  “Na leo,” kama mtu mmoja alivyoandika, “mtu huyu, William Branham, amekuwa na maelfu ya uthibitisho uliodhihirishwa kutoka kwa Mungu, na maisha yake yakiwa na mambo mengine yote yanayounda ofisi ya unabii, anapaswa kupokelewa – lazima apokelewe kwa jinsi alivyo.  “Bwana asema hivi” katika kinywa chake kwa Roho Mtakatifu, si tofauti kabisa na “Bwana asema hivi” katika kinywa cha Paulo, kwa maana ni Roho Mtakatifu yeye yule.

Lakini je, ungemtambua Paulo kama ungaliishi katika siku zake?  Au kama uliishi siku za Nuhu?  Au Eliya?  Au Yeremia?  Je! Ungewatambua kama manabii na kutii Ujumbe wao?  Vipi kama ungeishi sehemu ya mbali ya Palestina na kusikia taarifa kuhusu mtu anayeitwa Yesu ambaye alikuwa akifanya miujiza mikubwa?  Je! Ungemtambua kuwa Yeye ni nani, au ungekuwa kama Mafarisayo, ambao waliamini yale ambayo Mungu alifanya zamani, lakini hawakuweza kukubali kile ambacho Mungu alikuwa akifanya katika siku zao wenyewe!  Hata walimwita Yesu “Beelzebuli, mkuu wa mapepo”.  “Ole wenu, waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnayajenga makaburi ya manabii, na kuyapamba maziara ya wenye haki, na kusema, Kama sisi tungalikuwako zamani za baba zetu, hatungalishirikiana nao katika damu ya manabii. Hivi mwajishuhudia wenyewe, ya kwamba ninyi ni wana wao waliowaua manabii.”( Mt. 23:29-31 ).

UJUMBE WA MWISHO ULIOACHWA KWA SISI WOTE.

William Branham alikufa mnamo Desemba 1965 wakati gari lake lilipogongwa na dereva mlevi.  Kilikuwa ni kifo ambacho tayari alikitarajia kwa maono.  Lakini UJUMBE ambao Mungu alimtumia kuleta uhai hauwezi kufa.  Hivi leo kuna zaidi ya mahubiri 1,100 tofauti ya Ndugu BRANHAM yaliyorekodiwa kwenye kanda na mengi ya haya yamechapishwa katika mfumo wa vitabu vinavyozunguka dunia nzima, yakilia dhidi ya upotovu, yakiwaonya watu kwamba Yesu Kristo anakuja upesi sana, yakifunua ukweli kupitia Neno la Mungu, na kumwandaa Bibi-arusi kwa ajili ya Kuja kwa Pili kwa Yesu Kristo.  Ni “sauti ya mjumbe wa saba” na Ujumbe wa Neno wa mwisho kwa wakati wetu.

Mungu kwa mara nyingine tena ametembelea kizazi hiki cha mwisho kupitia nabii mkuu. Mtu mnyenyekevu, ambaye hakutamani umaarufu wala mali, ambaye hakukosa kamwe kutoa kila sehemu ya utukufu kwa Bwana Yesu Kristo.

Kwa kifupi makala hii imeonesha maisha yake, kwa ufupi na uthibitisho wake.  Hata hivyo, hii haijagusa hata Ujumbe alioleta, ingawa ni Ujumbe huo ndio muhimu zaidi.  Sasa ni juu yako kuchimba zaidi hazina hizi.  Vitabu na kanda zinapatikana endapo utahitaji, lakini lazima uwe mwaminifu kuchunguza, kupima uthibitisho, kulichunguza Neno, na kisha kuomba.  Kama ni Kweli, Mungu anakuhitaji uiamini.

Hatimaye Ndugu Branham alihitimisha: “Tuko mwishoni, marafiki.  Hivi karibuni wakati utaisha.  Mamilioni watapoteza maisha.  Mamilioni ambao sasa wanaamini kuwa wameokolewa watahesabiwa kuwa chakula wakati huu wa atomiki.  Tunaishi katika saa ya mwisho.  Kwa neema ya Mungu, kwa msaada wake tunazungumza na watu wake ili wapate kutazamia kuja kwake Kristo upesi…”

Pakua Pdf                                           

Soma Makala ya Kingereza hapa